02/04/2026
KWAHERI NDUGU WILLIAM LUKUVI, LAKINI CHUMVI IKIPOTEZA LADHA YAKE ITATIWA NINI HATA IKOLEE?
Mwl. John Pambalu
Kwanza nitoe pole kwa wote walioguswa na msiba wa Mzee Lukuvi. Pamoja na yote, bado tunabaki kuwa binadamu. Tukifanya k**a waliyotufanyia, atakosekana mwenye utu. Usipolipa baya kwa baya, ndipo utu unapobaki. “Rudisheni upanga arani mwake.” Lukuvi amekwenda. Wacha nizungumze na “Lukuvi” waliobaki. K**a chumvi ikipoteza ladha yake, itatiwa nini hata ikolee?
Ameondoka mshauri wa ndugu Samia. Ametuacha katika taifa ambalo wale waliowahi kusherehekea mateso na mauaji ya raia wasio na hatia, kwa majina ya wahaini au wakosoaji, leo hii nao wanapokumbwa na mauti au matatizo, umma unashangilia.
Ujumbe k**a “Asante Mungu kwa hiki kidogo”, “Kifo ni kifo”, au “Mungu amejibu” baada ya kifo cha mshirika au kiongozi wa serikali, kadiri vinavyozidi kusambaa, vinaonyesha wazi mpasuko mkubwa kati ya watawala na wanaotawaliwa.
Lakini je, hii ni kulipiza kisasi kwa Mungu? Kiimani, hapana. Maana Mungu alisema magugu na ngano vitaachwa vikue pamoja, na siku ya mwisho ndipo magugu yatafungwa kwa ajili ya moto na ngano kwa ajili ya ghala. Wema hufa, na wabaya pia hufa. Wema na wabaya wote huzeeka pia.
Lakini je, hali hii inatufundisha nini? Inatufundisha kuwa taifa limepoteza upendo, umoja na mshik**ano?
Naiona hatari mbele, tena hatari kubwa sana. Wanaosherehekea kifo cha Lukuvi leo, kuna “Lukuvi” mwingine yupo mtaa wa Kanyerere Butimba Mwanza, anaweza kuwa mjumbe wa shina au balozi wa nyumba kumi na mwingine yuko Namtumbo au Songwe. Usiniambie wataishia kusherehekea kifo cha Lukuvi wa Isimani na wasisherehekee cha Lukuvi wa Kanyerere. Hilo ni hatari zaidi.
Chuki hii ikizidi, itafikia hatua ya kumsaidia Mungu “kuvuna” vilivyo vyake. Na hapo, aliyesherehekea kifo na aliyeumia kwa kifo cha Lukuvi, hakuna atakayekuwa salama.
Lakini tumefikaje hapa?
1. Mauaji ya wakosoaji wa serikali
2. Utekaji wa watu wenye mawazo tofauti
3. Kesi za uongo dhidi ya wakosoaji
4. Kuumizwa kwa viongozi wa dini wenye mawazo tofauti
5. Kufungiwa makanisa na watumishi wa Mungu wenye mitazamo mbadala
6. Wizi wa kura na kunyimwa haki ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Haya na mengine mengi k**a haya yamelipasua taifa letu, lile tulilokuwa tunaimba, “Tazama ramani utaona nchi nzuri… Utumwa wa nchi Nyerere aliukomesha…”
Leo watu wamekuwa watumwa wa chuki, kutokana na uovu waliotendewa, waliosikia au walioshuhudia ukitendeka kwa ndugu zao umesababisha watu kujaa chuki. Nafikiri ni wakati wa kutafuta njia ya kutoka hapa tulipofika.
Nina ushauri muhimu kwa kila mwenye kulipenda taifa hili:
Futeni kesi za uongo. Lissu na Kaunya waachiwe huru. Fungulieni CHADEMA ifanye kazi zake. Ombeni radhi kwa yote yaliyotokea tangu 2015. Waliotesa, kuteka kuumiza na kuua watu wawajibishwe. Waliokimbia nchi warejee wakiwa na uhakika wa usalama na uhai wao.
Taifa liungane kuandika Katiba mpya yenye nguvu ya kudhibiti walafi na walevi wa madaraka. Hata Mungu atasema: “Wanangu wameamua kubadilika.”
Kila mmoja anaweza kuchagua kuwa chumvi. Chumvi huleta ladha, huzuia vitu kuharibika. Hata ikiwekwa kwenye kilichoanza kuharibika, hupunguza au kuzuia kuharibika zaidi.
Ninatamani kuona mtoto wa Mdude akicheza pamoja na mtoto wa Mchengerwa au Mwigulu. Lakini yote yanawezekana tu ikiwa kweli na haki vitarudi.
Mambo ya Mungu hayachunguziki. Unampiga risasi mtu. Unamnyima fedha za matibabu. Unamfunga kwa hila ili angalau afe kwa presha na hafi. Halafu anakufa anayekushauri kuyafanya au kutoyafanya unayoyafanya.
Mambo ya Mungu hayachunguziki jamani. Kifo ni mawaidha k**a ya Ramadhan na Kwaresma hayakutosha kuwaeleza acheni kuonea wasio na hatia. Wafungulieni mliowafungwa kwa hila. Ningetamani msome ule mfano wa Yesu juu ya yule mkulima aliyevuna vingi akaimbia nafsi yake ee nafsi yangu umepata vyote tunywe, tule na tufurahi. Yesu akaendelea kusema ee mpumbavu wewe ungejua leo wanaitaka roho yako.......
Ninasimama kwa zamu yangu kujenga palipobomoka. Wewe je?
Kwaheri Mzee Lukuvi. Ungesimama uone jinsi hata msiba wako haujatuunganisha bali umeongeza utengano. Kisha umshauri aliyekuteua ndipo uende. Lakini hilo haliwezekani tena.
Tumefika mahali ambapo hata mema machache uliyowahi kuyafanya leo hakuna yanayokumbukwa. Unakumbukwa kwa video zinazosambaa ambazo kwa upande wa ubinadamu wako ni kweli ulikosea kutamka maneno ya chuki dhidi ya waislamu wa Zanzibar na mzee Abuu wa Nela Mwanza?.
Kwamba mema uliyowahi kuyatenda, hakuna linalotrend hata moja. Tunayaona, tunayashuhudia na tunajiuliza tumefikaje huku?. Nenda Lukuvi tuliosalia bado tunayo nafasi ya kuwa chumvi au mwanga ili tuliponye taifa. Dua na sala yangu upate pumziko la amani.
“Nyinyi ni chumvi ya ulimwengu.”
Wasalamu,
John Pambalu
[email protected]