17/11/2025
Warsha Ya Mfumo Wa Tanzania Chamber Portal Yaendeshwa Kanda Ya Kaskazini*
Warsha ya mafunzo ya Mfumo Mpya wa Kidijitali – Tanzania Chamber Portal imezinduliwa rasmi jijini Arusha, ikiwa ni hatua muhimu katika safari ya mageuzi ya teknolojia ndani ya Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).
Akizungumza wakati wa ufunguzi kwa niaba ya Rais wa TCCIA, Mwenyekiti wa TCCIA Arusha Ndg. Walter Maeda alisema mfumo huu mpya utaongeza uwazi, ufanisi na kasi ya utoaji huduma kwa wanachama wa chemba na Wafanyabiashara nchi nzima.
Warsha hiyo ya siku nne imewakutanisha washiriki kutoka Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga ambao wanajengewa uwezo wa kutumia mfumo huo kwa usahihi kupitia timu ya wataalamu wa TCCIA kwa kupitia ufadhili wa (TMA).
Kwa mujibu wa Afisa TEHAMA wa TCCIA Florian Mihyo mafunzo haya yanafanyika kikanda ili kuhakikisha kila kanda inajengewa uelewa wa kutosha kabla ya uzinduzi rasmi. Mfumo huo utawezesha wanachama na wafanyabiashara wote kwa ujumla kupata kwa urahisi huduma k**a usajili wa uanachama, Cheti cha Uasili wa Bidhaa,Uwasilishaji wa Vikwazo visivyo vya Kiforodha kwa wafanyabiashara wanaopeleka bidhaa nje ya Nchi. Vilevile mfumo huu utakua dawati la huduma kwa wateja mtandaoni.
Washiriki wamepongeza hatua hiyo, wakisema itarahisisha biashara na kupunguza urasimu.
Bi. Frida Shedafa, Afisa Forodha II – TRA Namanga Mkoa wa Arusha amesema mfumo huo “utaimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma na Sekta binafsi, kupunguza urasimu na kuongeza uwazi, hasa kwenye maeneo ya mpakani k**a Namanga.”
Warsha hizi zinatarajiwa kuharakisha matumizi ya teknolojia ndani ya TCCIA na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa taifa.
*