08/05/2020
USIPOTEZE WATEJA WAKO KWASABABU YA Covid-19.
Virusi vya corona/COVID-19, vimetangazwa na Shirika la Afya Duniani kuwa ni janga kubwa lililoikumba dunia kwa sasa. Watafiti na wataalam mbalimbali wako katika hali ya sintofahamu na maswali mengi yasiyo na majibu sahihi huku wakiendelea na tafiti katika maabara zao kwa ajili ya uvumbuzi wa tiba ya kukabiliana na Covid-19. Janga hili limeleta athari nyingi katika nyanja mbalimbali zikiwemo shughuli za kijamii kusimama, watu kujitenga, ofisi za taasisi na mashirika mbalimbali kufungwa ili kuruhusu wafanyakazi wao wajikinge kwa kufanyia kazi nyumbani, mipaka ya viwanja vya ndege kufungwa n.k. Hali hii imesababisha biashara nyingi duniani kudorora na nyingine kufungwa. Kutokana na hali mbaya ya kibiashara katika wakati huu wa Covid-19, mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa Alibaba Group Bw. Jack Ma akashauri kuwa kwa wafanyabaishara, mwaka huu 2020 uwe mwaka wa kupigania sana kubaki salama na hiyo ndiyo itakua faida kwako.
Wateja waliokua wanafika kununua katika biashara yako kwa sasa wanatoka nyumbani kwa tahadhari kubwa na hawatakiwi kutembea kwa uhuru waliozoea. Ni ubunifu pekee na kuzingatia kubadilika kuendana na mahitaji na hali ya wateja kutakakokuwezesha kuendelea na biashara yako katika kipindi hiki cha Covid-19.
TAPBDS tunapenda kushauri wateja wetu na hata wafanyabiashara wengine kuchukua hatua na kuweka mipango madhubuti kwa haraka dhidi ya janga hili. Mojawapo ya eneo muhimu linaloathiriwa moja kwa moja na Covid-19 ni kudhorota kwa mahusiano na au kupoteza wateja. Ili hilo lisitokee, tunashauri kufanyika yafuatayo;
1. Pitia upya mipango uliyoiweka ya biashara. Tunatambua kila biashara inakuwa na mikakati aidha ya mwaka au miezi inayoongoza jinsi ya utendaji kwa kila siku. Sasa ili kwenda sambamba na hali hii, pitia upya mipango na mikakati uliyokuwa umejiwekea na uifanyie mabadiliko. Mabadiliko yafanywe kwa kuzingatia hali na mahitaji ya wateja kwa kipindi hiki. Mfano wa mabadiliko unayoweza kufanya ni kuhusu mbinu za kuwafikia wateja wako. K**a biashara yako inawahudumia wateja kwa kufuata huduma/bidhaa ilipo, sasa unaweza fikiria kuwafikishia mahali walipo, hususani majumbani mwao huku ukiwa umeweka tahadhari za kutosha kuepuka njia za maambukizi ya Covid-19.
2. Endelea kuwasiliana na wateja wako. Endeleza mawasiliano kwa ufanisi zaidi kwani hii ni njia pekee ya kudumisha mahusiano na wateja wako. Kwa hali ya kawaida mawasiliano hujenga uaminifu kati ya biashara yako na wateja wako. Fanya mawasiliano kupitia njia rafiki na sahihi k**a vile barua pepe,mitandao ya kijamii au simu ya mkononi. Hakikisha wateja wanapata taarifa ili wasibaki gizani. Endapo kuna huduma ambayo umeihairisha au umeisogeza mbelel sababu ya Covid-19, basi ni vyema wafahamishe. Na iwapo kuna bidhaa ambayo imekwama njiani au haitakamilika kwa wakati basi wajulishe na ikibidi warudishie fedha zao.
3. Tafuta taarifa. Ni muhimu kufuatilia kwa karibu taarifa kutoka kwenye mamlaka mbalimbali zinazosimamia biashara. Ipo kawaida ya hatua za usaidizi kuchukuliwa ili kuzisaidia biashara dhidi ya athari za majanga. Endapo unasikia chochote kuhusu hatua hizo basi fuata maelekezo ili unafaike au wasiliana nasi tukusaidie kuelewa undani wake. Ni dhahiri kuwa Covid-19 imegusa watu kiuchumi, kiafya na ustawi wao kiujumla. Sisi TAPBDS pamoja na wafanyabiashara wengine ni jukumu letu kuhakikisha tunakuwa salama na kuwasaidia wengine waendelee kuwa salama. Hivyo ni vyema kuwa na taarifa mbalimbali za kila siku juu ya mwenendo wa janga hili, jinsi ya kujikinga na kuepuka kuendeleza maambukizi.
Kwa usaidizi wasiliana nasi
Simu: +255222664619
Barua pepe: [email protected]
www.tapbds.com