03/10/2019
wizara_afyatz
Na WAMJW- DODOMA
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, imezifungia jumla ya maabara 13, ambazo ni sawa na asilimia 21% kati ya Maabara 61 zilizokaguliwa, huku ikitoa onyo kali kwa Maabara 48 kutokana na baadhi ya Maabara hizo kutokidhi viwango vya kutoa huduma za upimaji.
Hayo yamesemwa na Msajili wa Bodi ya Maabara Binafsi kutoka Wizara ya Afya Bw. Dominic John Fwiling'afu wakati wa ziara ya ukaguzi wa hali ya utoaji huduma za upimaji katika maabara zilizopo Jiji la Dodoma.
Amesema kuwa Bodi ya Maabara Binafsi katika kutekeleza majukumu yake, inaendeleza mpango wake wa kukagua Maabara Binafsi zote nchini ili kuhakikisha zinatoa huduma kulingana na miongozo ili kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Aliendelea kusema kuwa zoezi hilo limeanza Jijini Dodoma, huku lengo likiwa kukagua jumla ya Maabara 106 ili kujiridhisha utoaji huduma sahihi kwa wananchi, ikiwemo kukagua k**a Wataalamu waliopo wanakidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria.
Pia, Bw. Dominic Fwiling'afu amesema kuwa licha ya kukagua ili kujiridhisha na ubora wa huduma zinazotolewa na Maabara hizo, Bodi hiyo inajukumu la kuangalia ulipaji wa tozo mbali mbali uliowekwa kwa mujibu wa Sheria na kujiridhisha k**a Maabara hizo zimetimiza masharti wakati wa uanzishwaji wake.
Aidha, Bw. Dominic Fwiling'afu ameongeza kuwa, mbali na kuzifungia baadhi ya Maabara hizo ambazo hazijakidhi vigezo kulingana na Sheria na miongozo, Bodi imeendelea kutoa ushauri kwa wamiliki na Wataalamu wa Maabara ili kutoa huduma bora kwa Wananchi.
@ Dodoma, Tanzania