17/08/2018
HOJA ZA WENZETU WANAOHAMA CHAMA KIMOJA KWENDA KINGINE HAZIJITOSHELEZI.
Na Ndg. Eliud Kabamanya
WAKATI tukielekea katika siasa za ushindani nchini kwa maana ya kuwa na vyama vingi vyenye kuwa na sera mbadala na zaidi kuongoza katika kuchochea maendeleo ya nchi, taifa limekumbwa na zimwi la hama hama. Siasa za ushindani na vyama vingi ndiyo vichocheo vya maendeleo endelevu, kwa kuwa kupitia siasa hizo wananchi upata fursa ya kueleza, kuchangia, na kushirikisha wengine mawazo na mapendekezo yao juu ya maendeleo ya taifa husika. Na utaratibu huo uchagia kwa kiwango kikubwa kufikia maendeleo ya watu kwa ajili ya watu wenyewe. Kupitia mfumo huo wa siasa haijalishi chama ambacho mwananchi anakuwemo, bado anayo nafasi kubwa ya kuchagia katika maendeleo ya nchi yake.
Kwa siku hizi za karibuni tumeshuhudia wimbi la wanasiasa hasa wale wenye nyadhifa za uwakilishi k**a vile wabunge, madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa au wenyeviti wa vyama vya siasa katika ngazi za wilaya na mikoa, wakihama kutoka chama kimoja kwenda chama kingine. Pamoja na kuwa wapo waliohama kutoka CCM kwenda upinzani, wimbi hili la uhamiaji limewakumba hasa wanachama wa vyama vya upinzani wakitoka kwenye vyama vyao kwenda Chama Cha Mapinduzi. Hoja yao kubwa ni kuunga mkono jitihada za rais Dkt John Pombe Magufuli, kuwa ameonesha nia na uwezo mkubwa wa kutekeleza malengo na matamanio ya Watanzania kwa kiwango kikubwa.
Hoja yao ya pili ni kwamba katika vyama vyao hasa huko upinzani kuwa utawala wa vyama hivyo havizingatii misingi na kanuni za utawala wa sheria pamoja na misingi ya uanzishwaji wa vyama hivyo. Wapo wanao sema kuwa vyama vyao vimekuwa vikiongozwa kwa upendeleo na ukabaila, lakini pia wengine wemedai kuwa vyama vyao vimekuwa na ubadhirifu wa mali za vyama husika. Hoja hizi kwa kweli ni dhaifu hatuwezi kuzitumia kuthibitisha kuhama kwao. Na kwa maana nyingine tunaweza kusema ipo hoja zaidi ya hizo wanazozitaja
Pamoja na kuwa hizi hoja hazijitoshelezi hatukatai kuwa ni haki ya kikatiba ya kujiunga chama anachokitaka mtu ilimradi chama hicho kimesajiliwa halali na kinafanya shughuli za kisiasa kwa mujibu wa sheria na kanuni. Na ndio maana wakati wowote hatukuwahi kuhoji uhamiaji wa wanasiasa kutoka chama kimoja kwenda kingine. Lakini kwa sasa tunalazimika kuhoji hilo kwa sababu uhamaji wake ni sawa na safari ya nyumbu kutoka sehemu moja ya kwenda sehemu nyingine. Ziko sababu kadhaa ambazo tunaweza kuzitumia kujiridhisha kabisa kuwa hoja zinazotolewa na wanaohama vyama si za msingi bali ni zaidi ya wanachosema machoni pa wananchi kupitia vyombo vya habari.
Hoja ya kumuunga mkono Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kile anachokifanya, wahamaji wengi wanasema kuwa hii ndio sababu ya wao kuhamia Chama Cha Mapinduzi, kwa kuwa Rais huyo anatokana na chama hicho. Hoja hii ni mfu, kwa sababu nyingi mno, moja ni Rais Magufuli hatokani na Chama Cha Mapinduzi k**a wengi wanavyodhani. Rais wa Jamhuri ya Muungano anapatikana kwa njia ya kugombea na kupigiwa kura na wananchi wote. Pamoja na kuwa anatakiwa awe na chama cha kupitia lakini bado anapigiwa kura na wananchi wote. Kwa lugha Rais ni mwananchama wa chama fulani aliyekubaliwa na wananchi kusaidiana nao kwa wakati wa kipindi cha miaka mitano kutekeleza malengo na matamanio ya wananchi. Kwa hiyo ni jukumu la watanzania wote wapenda maendeleo walioko ndani ya chama chake au nje ya chama chake kumuunga mkono. Tuelewane jambo moja kumuunga mkono Rais haina maana kwamba umshangilie anapofanya jambo jema. Hata kumkosoa anapokosea ni kumuunga mkono, mfano Tanzania wakati fulani ilikuwa na mjadala juu ya kusaini mkataba wa kushirikiana na Umoja wa Ulaya katika biashara (EPA) Watanzania wote walijaribu kutoa hoja zao na mawazo yao juu ya waonavyo kuhusu jambo hilo. Kwa muundo huo walikuwa wanamuunga mkono kiongozi wao katika utekelezaji wa shughuli zake. Mfano mwingine ni pale wanapohoji kutoheshimu katiba, jambo hili halifanyiki kwa maana ya kumpinga Rais bali ni kumkumbusha makubaliano ya Watanzania kwa ujumla, Kazi hii haikutaki uhamie kwenye chama chake bali umakini na ufundi wa kueleza jambo ambalo unafikiri linaweza kufanyika kwa maslahi mapana ya taifa.
Jambo la pili ni la kitakwimu, sote tunakumbuka kuwa Mheshimiwa Rais Magufuli amepatikana kwa kupata kura zaidi ya 58% ya wapiga kura wote, waliokuwa wamejiandikisha kupiga kura mwaka 2015. Waliojindikisha ni ni zaidi ya milioni sita mpaka nane ambazo ndizo zilikuwa zinakadiriwa kuwa wananchama wa Chama Cha Mapinduzi wakati huo. Viwango hivyo vinakuonyesha kabisa kuwa Mheshimiwa Rais Magufuli ametokana na wananchi kupitia chama cha siasa, maana yake haikulazimu mwanasiasa kujiunga na chama chake ndo useme unamuunga mkono wakati pengine ulimpingia kura ili awe rais wa Jamhuri ya Muungano.
Tatu, wakati Rais Magufuli ametembelea chuo kikuu cha Dar es Salaam mapema mwaka 2016 nakumbuka alimtaja Dkt (Prof) Kitila kuwa ni mwanasiasa wa mfano kwa maana anaweza kueleza mapungufu na mema ya serikali hata k**a hayuko ndani ya chama chake. Maneno hayo ya Mheshimiwa Rais yanatosha kuthibitishia kuwa hatuhitaji kujiunga na chama chake ili kumuunga mkono. Yanaonyesha wazi wazi kuwa bado mtu ang’e weza kummunga mkono akiwa nje ya chama chake, na bado mambo yakaenda sawa.
Nne ni kuhusu itikadi za chama na utamaduni wa chama, wote tunajua kuwa chama cha siasa kwa namna yoyote hile lazima kiwe na itikadi na utamaduni unaokiendesha. Mfano Chama Cha Mapinduzi itikadi yao hadi sasa wanajinasibisha na siasa za kijamaa na Kujitegemea. Vyama vingine navyo vinaitikadi zake. Mtu anapotaka kujiunga chama cha siasa kwa malengo ya kukisaidia chama husika kwanza ni lazima akubali itikadi ya chama anachotaka kuhamia. Kwa maana, k**a ameikubali na kuielewa itikadi ya chama hicho basi atakuwa mfuasi na mtetezi mzuri wa itikadi husika. Jambo ambalo ni nadra sana kulisikia katika hotuba za wanaohama vyama. Kila anayehama utasikia anasema ana muunga mkono Rais kwa juhudi zake za kusimamia uwajibikaji, na kujitahidi kuleta maendeleo. Hakuna anayetaja kuwa amevutiwa na itikadi anayosimamia Mheshimiwa Rais na chama chake. Hali hiyo inaweza kutufanya kufikiri ama wanayemuunga mkono hana itikadi au wao wenyewe hajajishughulisha kujua itikadi ya chama wanachohamia. Na k**a hivyo ndivyo basi hatuna budi kuwaona watu hao wakihama chama hicho kwenda vyama vingine, kwa kuwa hawana wanachoamini.
Tano, Urais na nchi hizi ni taasisi zinazotakiwa kujisimamia sio kutegemea mtu, mfano mtu anayepewa wajibu wa kusimamia taasisi ya Urais muda wake ni vipindi viwili vya miaka mitano tu k**a ataweza kuchaguliwa katika vipindi hivyo. Kwa upande wa pili nchi ni taasisi inayodumu kwa manufaa ya wananchi kwa muda wote. Kwa mantiki hiyo hatutakiwa kujiunga na chama chochote kwa kumuunga mkono kiongozi wa chama husika. Tunachotakiwa kuunga mkono ni maendeleo na Ustawi wa nchi kwa ujumla. Rais awezi kukaa madarakani milele anakaa kipindi chake kikiisha anatakiwa kurudia nafasi yake ya uraia mwenye sifa ya kuwa Rais Mstaafu. Hivyo si kazi yetu kuunga mkono pale anapokuwa anatekeleza wajibu wake. Lakini pia k**a tunamuunga mkono k**a yeye bila kujua jukumu lake ni nini, maana yake hatujifikirishi kujua je k**a atamaliza muda wake je tutahama chama chake kwa kuwa hatuna wa kumuunga mkono, au tutafuta namna ya kuondokana na nchi yetu. Kwa maana tumejikita katika kuunga mkono mtu binafsi sio nchi au Urais.
Hoja ya ukabila na kutozingatia utawala wa sheria katika vyama walivyokuwemo, hoja hii pia inaweza kupingwa kwa sababu za kihistoria na kisiasa. Hoja ya kihistoria inatuonyesha kuwa waliohama wengi si tu walikuwa ndani ya vyama hivyo awali bali pia walitoka katika chama wanachorudi leo. K**a hivyo ndivyo je huko waliko kuwa awali kulikuwako ukabila na utawala usiozingatia misingi? Je leo kumebadiliaka? Tukiachilia hilo utaona kuwa wote wanaosema ukabila na kutozingatia utawala wa sheria, watu hao waliowengi wamepata ubunge wakiwa huko, wamepata udiwani wakiwa huko na mengine mengi yaliyowanufaisha sana. Sasa wakati huo wanapata nyadhifa na vyeo ukabila huo na utawala usiozingatia taratibu hakuwepo? Na k**a ulikuwepo ni Jitihada zipi walifanya kuhakikisha jambo hilo linaodolewa? K**a hawakufanya jitihada je wanaweza kuturidhisha kuwa wamechangia katika kututengenezea bomu linaloweza kulipuka hapo baadae? Kwa sababu k**a sehemu kuna siasa za ukabila na wewe umeziacha ziendelee kuchanua maana yake umeacha siku moja taifa ligawanyike kwa misingi hiyo ya kikabila.
Si jambo la afya hata kidogo kwa siasa zetu tuapohama vyama vyetu kwa hoja ya kuunga mkono Rais, tunadidimiza itikadi na ukuwaji wa vyama vya saisa.
Mwisho.