17/08/2026
WAZIRI KABUDI ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA ASA CHINI YA PROGRAMU YA AFDP
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, ameridhishwa na utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), inayofadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).
Amesema hayo wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi katika Shamba la Mbegu la Kilimi, Nzega–Tabora, Agosti 17, mwaka huu. Amesema utekelezaji wa miradi hiyo umeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo kwenye mashamba ya ASA, hasa kwa kuongeza uzalishaji wa mbegu.
Katika ziara hiyo, Waziri Kabudi amekagua miradi inayotekelezwa na ASA kupitia AFDP ikiwemo Ujenzi wa Jengo la Utawala, Ujenzi wa Jengo la kukaushia Mbegu, Ujenzi wa Nyumba za Watumishi, pamoja na shughuli za uzalishaji wa Mbegu.
Waziri Prof. Kabudi amesema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ya AFDP ili kuhakikisha inafanyika vizuri.
Aidha, Waziri Kabudi alipata fursa ya kukagua miundombinu ya umwagiliaji katika shamba hilo na kujionea kilimo cha kisasa cha mifumo ya umwagiliaji ambacho kimebadilisha sura ya uzalishaji wa mbegu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, amesema Wizara inaendelea kusimamia vizuri miradi ya ASA inayotekelezwa kupitia AFDP kwa kufuata taratibu zote za Serikali.
Amesema majengo na vifaa vilivyokaguliwa na Prof. Kabudi vimesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji wa mbegu kwa ASA.
Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuhakikisha miradi yote inaleta tija kwa jamii.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Mhandisi Innocent Masaka, amesema maoni yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi kwa uzito unaostahili.
Mhandisi Masaka amesema Shamba la Mbegu la Kilimi, kupitia Programu ya AFDP, linaendelea kuwekewa miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa ghala la kuhifadhia mbegu, kusimika mtambo wa kuchakata mbegu, na ununuzi wa vifaa vya karakana, ambapo miradi hiyo itatumia jumla ya Shilingi bilioni 5.5 katika shamba hilo.