05/02/2026
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Same limepitisha mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027 wenye jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 60.3, hatua inayolenga kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Bajeti hiyo imepitishwa katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Februari 04, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Same.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Bw. Yusto Mapande, alisema kuwa bajeti hiyo imelenga ustawi wa wananchi wa Same kwa kuzingatia mahitaji yao ya msingi na vipaumbele vya maendeleo.
Alieleza kuwa bajeti hiyo imejikita katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo sekta za afya na elimu, ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Same, uendeshaji wa halmashauri, ujenzi wa uwanja wa michezo pamoja na kuboresha miundombinu mingine ya kimaendeleo ili kukuza uchumi wa wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, alitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa madiwani kuhusu umuhimu wa wananchi kujiunga na bima ya afya kwa wote, Aliwataka madiwani kuhakikisha wanawaelimisha wananchi kuhusu faida za bima ya afya kwa wote ili kuwawezesha kupata huduma bora na za uhakika za matibabu.
Aidha, alipongeza kupitishwa kwa bajeti hiyo na kusisitiza umuhimu wa usimamizi mzuri wa fedha za umma ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kasilda aliwasisitiza madiwani na watumishi wote wa umma kuhakikisha wanawaelimisha wananchi na kuhamasisha utunzaji wa mazingira pamoja na upandaji wa miti, hususan miti ya matunda, ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same, Bw. Abdallah Mnyambo, aliwasisitiza watumishi wa umma pamoja na viongozi wa serikali kusimamia ipasavyo miradi na miundombinu yote ya kimaendeleo ili idumu kwa muda mrefu na kuepusha uharibifu wa rasilimali za umma.