26/08/2026
ZEC YAPATA USHINDI MAJIMBO TISA YA UCHAGUZI
Mahkama Kuu ya Zanzibar imetupilia mbali maombi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi wa Uwakilishi wa mwaka 2025 yaliyowasilishwa na Chama cha ACT Wazalendo katika majimbo tisa ya Tumbatu, Kijini, Bumbwini, Amani, Mwera, Mtoni, Welezo, Nungwi na Mpendae.
Maombi hayo yameondolewa baada ya Mahkama Kuu, chini ya Jaji Salma Ali Hassan, kusikiliza na kuamua juu ya Pingamizi za Awali zilizowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wanasheria kutoka Afisi ya Tume Ya Uchaguzi ya Zanzibar wanaowawakilihsa Wasimamizi wa Uchaguzi wa majimbo hayo.
Pingamizi hizo za awali ziliwasilishwa na waombewa "Respondants" katika kesi hizo wakipinga namna maombi hayo yalivyowasilishwa, hali iliyosababisha Mahkama kuyazingatia Pingamizi hizo kabla ya kuendelea na usikilizwaji wa mashauri hayo kwa msingi wa hoja za uchaguzi.
Katika uamuzi wake, Mahkama Kuu imeamua kuyatupilia mbali maombi hayo, hatua inayomaanisha kuwa malalamiko yaliyowasilishwa na ACT Wazalendo katika majimbo hayo tisa hayataendelea kusikilizwa kwa misingi iliyowasilishwa katika maombi hayo.
Majimbo yaliyohusika katika maamuzi hayo ni Tumbatu, Kijini, Bumbwini, Amani, Mwera, Mtoni, Welezo, Nungwi na Mpendae.
Uamuzi huo ni miongoni mwa hatua za kisheria zinazohusiana na mashauri ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2025, ambapo baadhi ya Wagombea na Chama cha ACT-Wazalendo walipoamua kuchukua hatua za kisheria kupinga matokeo ya Uchaguzi wa Wawakilishi yaliyotangazwa katika Majimbo hayo